By FD Ninga, CBNRM Programmes Coordinator, TNRF
Tarehe 24-02-2016 Jumuiko la Maliasili Tanzania lilishiriki na kuchangia mijadala kwenye mkutano wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania (SHIVIMITA), uliofanyika katika ukumbi wa Hazina, Dodoma. SHIVIMITA ni chombo kikuu cha sekta binafsi kitaifa yaani “national overall apex - level Private Sector Organisation (PSO)” katika Sekta ya Misitu na Viwanda vya Misitu nchini. SHIVIMITA ipo kwa niaba ya wawekezaji binafsi wote nchini, waliowekeza katika nyanja zote za sekta ya misitu.
Mgeni Rasmi wa mkutano huo alikuwa ni Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii - Mhandisi Ramol Makani. Mkutano ulilenga katika kuangalia namna za kuimarisha uwekezaji, ufanisi na taasisi binafsi katika tasinia ya misitu ili kukuza uchumi wa Taifa (Strengthening Investment, Efficiency and Private Sector Institutions in Forest Industry Sector, for Expedited National Economic Growth).
Ushiriki wa Jumuiko la Maliasili, ukiwakilishwa na mratibu wa miradi ya usimamizi wa maliasili wa jamii Bwn. Faustine Ninga, aliyeambatana na wawakilishi watatu wa wafanyabiashara wa mbao/magogo na mkaa (Frank Nganyanyuka, Hassan J. Kilungi, na Saidi Yusuph) ulikuwa na lengo la kuchangia mijadala, lakini pia kuwasilisha maazimio yatokanayo na midahalo ya wafanyabiashra. Ikumbukwe kuwa, Jumuiko la Maliasili Tanzania, kupitia programu yake ya ushirika na WWF Tanzania inayohusu mambo ya ‘Uwekezaji katika Misitu na Ardhi’ inayofadhiliwa na WWF Finland, pamoja na Programu ya “Mama Misitu Campaign” inayofadhiliwa na Serikali ya Finland, limekuwa likijihusisha na wafanyabiashara wadogo wadogo wa mazao ya misitu, na hasa mbao, magogo na mkaa ili kuhamasisha biashara iliyo halali, kupunguza migogoro, na kufuata taratibu na sheria za nchi. Mijadala ya hivi karibuni imelenga katika kuimarisha vyama vya wilaya vya wafanyabiasha wa mazao ya misitu ili kujenga jukwaa la kupashana habari, kuratibu mambo mbalimbali na kujadili changamoto zinazoikabili tasinia hiyo. Katika jitihada hizo, Jumuiko la Maliasili liliandaa mkutano wa kanda ya kusini, uliojumuisha wafanyabiashara wa mbao na magogo wa uwanda wa Selous-Ruvuma siku ya tarehe 19-02-206 Mkoani Lindi. Maazimio ya mkutano huo yanapatikana katika tovuti ya Jumuiko, bofya hapa: http://www.tnrf.org/en/content/yaliyojiri-katika-warsha-ya-wafanyabiashara-wa-mbaomagogo-wa-uwanda-wa-selous-ruvuma-tarehe
Hivyo, ushiriki wa Jumuiko katika mkutano wa SHIVIMITA ulilenga katika kuwasilisha maazimio hayo na kuona namna bora ambayo vyama vya wafanyabiashara vinaweza kuwakilishwa na kuunganishwa katika chombo kikubwa cha kitaifa, yaani SHIVIMITA.
Kwa taarifa zaidi, nimeambatanisha katika andiko hili: risala kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na mawasilisho mbalimbali.
Attachment | Size |
---|---|
risala_kwa_dep._minister_wmu_na_serikali_feb_24_2016_dom_mtg.doc | 59.5 KB |
presentation_uvunaji_februari_2-_3.ppt | 183 KB |
ttcs_wasilisho_shivimita_dodoma.ppt | 8.07 MB |
dodoma_presentation.pptx | 19.37 MB |